|
|
|
![]() ![]() |
||
|
Gazeti INJILI Kwenye Internet - http://www.munishi.com Tel. 254-722-602445 E-mail: munishi@munishi.com Wazo
La wiki Baada ya Kibaki kuchukua hatamu za uongozi Kenya, Ahadi nyingi walizoahidi wakati wa kampeni bado hawajatimiza. Katiba waliyoahidi kuibadili siku mia moja za kwanza mdarakani, bado haijakuwa tayari. Kila dalili zinaonyesha kwamba Kibaki hataki katiba mpya itakayompunguzia madaraka. Tunachokishuhudia sasa ni kamati za kuchunguza kamati itakayochunguza kama katiba mpya inatakiwa. Wengi wanaliona hilo kama kupoteza muda wakati nia ya kuweka katiba mpya haiko kwa Kibaki. Wanasema hiyo ndiyo siasa. Kudanganyana mchana kweupe, Jua likiwaka? Vyama 15 ambavyo ndivyo vinavyojumuisha muungano wa Narc National Reimbow coalition, vilikutana chini ya uenyekiti wa rais Kibaki kujadili mzozo uliojitokeza katika chama hicho. Utata ulizuka pale wanachama wa muungano huo walipoambiwa kwamba wavifute vyama vyao na badala yake wajiunge na chama kimoja cha Narc ifikapo desember mwaka huu. Wengi walisema kwamba enzi ya chama kimoja ilipita kitambo, na kuwarudisha kwenye enzi hizo ni sawa na ndoto za mchana. Chama cha kwanza kupinga pendekezo hilo ni LDP. Walisema siku za kuongozwa kidicteta zilikwisha. Pia walisema kwamba hawakujiunga na Narc ili wamezwe bali kuunda muungano utakaolinda maslahi ya kila chama. Kwamba walisema Kibaki mwanachama wa DP anatosha, haikumaanisha wamezwe na DP kwa jina jipya la Narc. waliongeza kwamba Narc itabaki muungano wa vyama, na itakuwa imara kama makubaliano yaliyowaunganisha yatafuatwa. Vinginevyo walisema hapana hawatakubali. Nalo gazeti la NATION likiripoti habari hizi kwenye ukurasa wake wa mbele lilisema "Narc kuungana kama chama kimoja mwishoni mwa mwaka." Kwao hawakuziona tofauti zilizojitokeza mkutanoni, jambo linaloashiria kwamba gazeti hilo linaunga mkono vyama vingine kumezwa na DP kwa jina jipya la Narc. Ndiyo maana watu wengi siku hizi husoma Standars na Kenya Times kwa habari sahihi. Kwamba vyombo vya habari vitakubali kutumiwa kuturudisha kwenye utawala wa kiimla hilo linatisha. Redio injili Fm itasimamia haki daima. Usikose kuisikiliza kwa habari sahihi. unaendelea kuisikiliza taarifa ya habari kutoka redio injili fm, inayokutangazia ulimwenguni kote kwenye masafa ya Internet www.munishi .com/ redio injilifm Wanasiasa huchaguliwa na wananchi ili waingie bungeni kutunga sheria. Wakisha fanya hivyo, Sheria inapaswa kuwa kama msumeno unaoweza kuwakata hata wanasiasa wenyewe. Inapotokea kwamba wanasiasa ndio wanaoongoza katika kuzivunja sheria, wanategemea nani katika jamii azitii sheria? Inasikitisha tunapowaona wanasiasa Afrika wakiunda kamati za kuwachunguza wafisadi katika taasisi mbalimbali, na wanasahau kuichunguza taasisi yao ya siasa ambayo imeoza kwa maovu ya kila aina. Kuanzia mauaji ya kisiasa ufisadi, Uongo ulio wazi, pamoja na unafiki. Wanapambana na ufisadi siyo kwa sababu wanauchukia, bali wanafanya hivyo baada ya kuwekewa shinikizo na mataifa ya magharibi na hasa Amerika. Ndio maana ufisadi kumalizika Afrika ni sawa na ndoto za mchana. Wanaojaribu kupambana na ufisadi wanafanya hivyo baada ya kuamrishwa na Amerika ambao nao ni wafisadi nambari moja. Waamerika wakitaka kuanzisha chochote katika nchi za wenyewe, wako tayari kutoa chochote ili wafanikiwe. Je huo siyo ufisadi? Nchini Tanzania wamenunua kila kitu. Wanatumia lugha ya ubinafsishaji kufanikisha malengo yao. Mashirika yote ambayo ni uti wa mgongo wa uchumi wa nchi nyingi Afrika yako mikononi mwa makampuni ya nchi za magharibi na Amerika ndiyo inayoongoza katika hilo. Inatia kichefuchefu tunapowasikia viongozi Afrika wakiwasha moto wa mabua kupambana na ufisadi kiunafiki. Moto wa namna hiyo huzimika mara wanapopewa walichoahidiwa. Wakati umefika kwa viongozi wa kidini kuunda kamati za kuwachunguza viongozi Afrika. Wawafundishe kuzichukia dhambi kwa dhati, na wapambane nazo kwa sababu wanazichukia na siyo unafiki wa kushinikizwa na ahadi za misaada kutoka Amerika. Kinyume cha hayo, wasitegemee kwamba kuna mtu atakayetii sheria ambazo wenyewe wanazivunja. Ikiwa wanasiasa wanawezakubaliana jambo mbele ya mwanasheria, halafu baadaye wakiuke makubaliano, Mnategemea wanasheria kuheshimu sheria? Ndio maana vyombo vya sheria haviheshimu sheria. Siasa inapokuwa sheria, na sheria kuwa siasa wananchi tuko hatarini. Nasikitika kusema kwamba katika nchi zetu za Kiafrika kila kitu ni siasa na siasa ni kila kitu. Ndiyo maana hatua za haraka lazima zichukuliwe kutenganisha siasa na maisha yetu. Tuwe na mahali pa kumuomba Mungu na kuzitii sheria zake bila siasa. Rais anapotumia nguvu za katiba ya zamani kuwasimamisha kazi majaji waliomwapisha aingie ofisini, ni wakati wa majaji hao kumkumbusha kwamba aliahidi kuweka katiba mpya baada ya siku mia moja. Wakishindwa kumuuliza, waombe msaada wa maaskofu, waunde kamati ya kumchunguza. Kamati zimekuwa nyingi, na kinachohitajika sasa ni kamati za kuchunguza kamati. Kabla ya kamati za kuchunguza kamati kuundwa, msisahau kuunda kamati ya kuvichunguza vyombo vya habari. Mchango wao katika kuwasaidia wanasiasa kuendeleza maovu katika jamii. Kamati zitakapokuwa nyingi, itabidi na zenyewe zichunguzwe na kamati zitakazopeleka ripoti kwa kamati zinazochunguza kamati. Majaji wanaosemekana wafisadi, waliwahi kuwahukumu wengi waende jela, na wengine walihukumiwa vifo. Kwa kuwa imegundulika walikuwa wafisadi kesi walizohukumu awali zitarudiwa ili haki itendeke? Mtafanyaje na wale waliohukumiwa kifo na majaji hao? Huwezi kuisafisha bahari kabla ya kusafisha mito michafu inayoleta maji baharini. Kufanya hivyo ni sawa na kujaribu kuukimbiza upepo. Wanasiasa waache kutudanganya. Wao ndio wamehujumu uchumi. Wakirudisha pesa zote walizojipatia kwa njia za ufisadi, uchumi utarekebika ili watumishi wa umma wapewe mishahara ya kuwatosha. Ni kweli kwamba hakuna pesa zinazoweza kumtosha mwanadamu, lakini angalau mishahara yao itoshe kumudu maisha ya kila siku. Ikiwa mishahara haitoshi chakula, mnategemea nini kutoka kwa watumishi kama hao? Rushwa ni mbaya na siwezi kuwatetea wafisadi. Lakini wafisadi hawawezi kuumaliza ufisadi. Kupambana na ufisadi ni hatua nzuri. Kufanya hivyo ili kuwaridhisha Amerika wafisadi mambari moja, ni vibaya sana. Hatua nzuri ikichukuliwa kwa lengo baya, inaharibu kila kitu. Mwisho hata hatua yenyewe inakuwa mbovu. Wito umetolewa kwa viongozi Afrika kuimarisha huduma za afya nchini mwao. Gharama za matibabu katika bara letu ni za juu kiasi kwamba wananchi wengi wanashindwa kumudu. Viongozi Afrika hawafanyi juhudi kuboresha mahospitali badala yake hujilimbikizia pesa za kutibiwa ngambo endapo wataugua. Pamoja na jitihada za viongozi wengi Afrika kujipenda kuliko wananchi wanaowaongoza, Wengi walioenda kupata matibabu ngambo walirudi maiti. Nyerere na Mobutu ni mfano wa viongozi waliotumia pesa nyingi kutibiwa nje ya Afrika lakini bado mauti iliwaita. Kenyatta Rais wa kwanza Kenya alikataa kata kata kupelekwa ngambo kutibiwa. Pamoja na mambo mengine hakuwaamini madaktari wa nchi za magharibi. Alihoji kama watu wametutawala na wameondoka shingo upande, nini kitawazuia kummalizia kiongozi mgonjwa wa bara hili wakati atakapokataa kusaini mkataba wa kuyauza mashirika yetu kwa makampuni yao ili waendelee kutunyonya? Aliongeza kwamba wakoloni watautumia ugonjwa wa kiongozi wetu kama mtego wa kunasa panya. Siyo ajabu akaambiwa auze sehemu ya nchi iwe kambi za kijeshi za taifa linalompa matibabu. Wananchi wengi Afrika walimpenda Kenyatta kwa msimamo huo. Aliwaamini madaktari wa kiafrika, na alifanya kila juhudi kuwasomesha ili waitumie taaluma yao barani Afrika. Leo hii madaktari wetu wanaikimbia Afrika kulipwa pesa nyingi nchi za magharibi. Kwao pamoja na viongozi wanaojipenda, tunasema AIBU KWENU. Wananchi tunasema Mungu atatusaidia. Imani yetu kwake itatuponya hata kama tutatafuna majani ya miti kama dawa. Anayaona mateso yetu, na anaona jinsi viongozi wanavyojipenda wenyewe. Atahakikisha kwamba wakienda ngambo kutibiwa wakiwa moto, watarudi Afrika wakiwa baridi. Lakini wakitaka laana hii iwaondokee, waanze sasa kuziipa kipau mbele huduma za afya katika nchi zao. Mmoja kati viongozi wa tume ya kurekebisha katiba, ameuawa kwa kupigwa risasi. Daktari Othiambo Mbai ambaye pia ni mkufunzi katika chuo kikuu cha Nairobi alishambuliwa nyumbani kwake na watu wenye silaha. Majirani walimkimbiza Nairobi Hospital ambako aliaga dunia alipokuwa akifanyiwa upasuaji kuondoa risasi nne mwilini mwake. Kulingana na madaktari waliomfanyia upasuaji, Daktari mbai alikuwa na majeraha ya risasi kichwani mkononi tumboni na kwenye paja. Inaonekana kwamba wauaji wake walikuwa wamekuja kufanya kazi moja tu. Nayo ni kumuua Daktari Othiambo Mbai. Akiongea na waandishi wa habari hospitalini, Mheshimiwa Raila Odinga alisema kwamba mauaji ya Daktari Mbai ni mauaji ya kisiasa. Naye Profesa Yash Pal Ghai alisema kwamba inaonekana kwamba wauaji walikuwa wamekodishwa kufanya kazi hiyo. Lakini naibu mkuu wa polisi Nairobi bwana Nicodemas Diffu alisema wanayachukulia mauaji hayo kama uhalifu wa kawaida mpaka ushahidi wa aina nyingine upatikane. Alipoulizwa kwamba waliupata wapi ushahidi kwamba hao walikuwa wahalifu wa kawaida alisema bado wanafanya uchunguzi. Siasa ni siasa. Yaani kitu ambacho siyo chenyewe hasa. Ikiwa Mwanasiasa anaweza kumdanganya mwanasiasa mwenzake mchana jua linawaka, bila kujali kwamba makubaliano yao waliandikiana kwa wakili, vipi kuhusu ahadi walizotuahidi wananchi bila maandishi yeyote? Inapokuwa wazi kwamba wanasiasa wanaweza danganyana, ndipo wananchi tunapofunguka macho. Kwa vyovyote lazima tumuonee huruma aliyedanganywa hata kama kwa sasa hana la kufanya. Bila kujua, huyo aliyedanganya amejipunguzia heshima yake kisiasa na kidini. Alisaidiwa na sasa haoni kama alisaidiwa. Msemo wa kiswahili kwamba shukrani ya punda ni mateke sasa unamaanisha kwa wengi. Yale yaliyotajajiwa na wengi, sasa yametimia. Imekuwa wazi kwamba viongozi walio madarakani hawana haraka ya kuirekebisha katiba. Wanadai kwamba ile ya zamani ndiyo waliyoaapa kuilinda na kuitetea. Mbaya zaidi wanasemea kanisani mahali ambapo ukweli ulipaswa kutiliwa maanani. Itakumbukwa kwamba wakati wa uchaguzi mkuu uliomalizika, ahadi nyingi zilitolewa na moja ikiwa ni kuhakikisha katiba mpya imeidhinishwa baada ya siku mia moja za uongozi mpya. Pamoja na mambo mengine katiba mpya ilipaswa kuwa na vipengele vinavyopunguza madaraka ya rais ili asiyatumie vibaya kama waliomtangulia. Na hapo ndipo suala la waziri mkuu lilipochipukia. Lakini mambo yalivyo sasa inaelekea kwamba harakati za ukombozi ndio kwanza zinaanza. Kwa wananchi mambo yanaelekea kuwa kama yalivyokuwa kama siyo mabaya zaidi ya ilivyokuwa. Ushwari wa kisiasa ulioonekana kipindi chote cha mwanzo umeanza kupata mbadala wake ambaye ni maandamano ya wanafunzi wanaobeba mabango yaliyoandikwa MoU yakimaanisha Memorandan of Understanding, au Makubaliano ya awali. Ilianzia kwenye mazishi ya Wamalwa ambapo Polisi wa kutuliza ghasia walikabiliana na wanafunzi hao vilivyo. Yote haya ni ya nini? Serikali ya haki, Polisi wake wa kutuliza ghasia wanakuwa kambini siku zote. Ukishaanza kuwaona mitaani na hata kwenye mazishi, ujue kuna majambo hayaendi vizuri na nguvu inatumika kunyamazisha mambo. Nguvu inaweza kunyamazisha jambo kwa muda, lakini haiwezi kulizuia lisitokee hata kama itachukua muda gani. KANU walitumia nguvu kupita kiasi kuzuia mabadiliko, lakini hatimaye yalitokea na sasa wako nje ya madaraka. Walioko madarakani wakisahau waanze kuyazuia mabadiliko yaliyotarajiwa yasitokee, watajikuta wakinyolewa na wembe walioutumia kuinyao KANU. Mungu ibariki Kenya. Bariki na Tanzania, Tena uisaidie nchi ya Tanzania iweze kuyafikia mabadiliko hatua ya kwanza kama yaliyotokea Kenya. Viongozi Kenya wasaidie wasijisahau mapema kutimiza ahadi walizowaahidi wananchi mbele yako. Uliwasikia wakiahidi na wasaidie wayatimize yote waliyoahidi ili Kenya iwe mfano mwema wa kuigwa Afrika. Nairobi Ufisadi bado ni maji marefu yanayotishia kuzamisha wengi. Ila tunatoa pongezi zetu kwa viongozi wa serikali mpya kwani mabadiliko mengi yameanza kuonekana. Sasa unaweza kuhudumiwa katika ofisi za serikali bila kutoa kitu kidogo. Waliahidi kupigana na ufisadi na na matunda tumeanza kuyaona. Lakini haimaanishi kwamba ufisadi umeisha kabisa. Ndio maana siyo busara kupuuzia kelele zinazopigwa na baadhi ya viongozi kwamba dalili za ufisadi zimeanza kuonekana. Mtu msafi akionyeshwa doa kwenye nguo yake atafurahi ili aliondoe abaki msafi. Ila akibisha kwamba hakuna doa nasi tunaliona, basi yatakuja madoa mengi mpaka rangi ya nguo itapotelea kwenye madoa Mtu akikosa adabu, Hafundishwi adabu kwa kukosewa adabu. Tena mtu akiiba, adhabu yake siyo kuibiwa. Mwizi anaweza kutuonyesha mwizi kwa sababu wanajuana. Mkisema yeye ni mwizi na hafai kuwaonyesha nani anayewaibia, Basi mtaibiwa sana. Na kitambo mjue kwamba mnaibiwa, mtakuwa mmechelewa sana. Waacheni watuambie nani anayetuibia, Kwani ni kosa kufikiri kwamba serikali mpya haiwezi kuwa na wezi wa mali za umma. Wengi walihusika na yote yaliyotufika katika serikali za awali. Nini kitawafanya wasiyarudie waliyoyazoea? Au walitubu? Sikuwasikia wakitubu, bali walihama kwenye jahazi lililokuwa likizama na wakajisalimisha kwenye meli ya Narc iliyokuwa inakaribia kungoa nanga. Kwangu niliwaona kama watu waliojisalimisha wenyewe wasizame siyo kwamba walikuja kutuokoa tusizame. Wananchi bado maji yako shingoni. Maisha bado ni magumu. Pesa hazipatikani kirahisi. Zikipatikana matumizi yake ni mengi wala hazitoshi. Kazi hakuna, Na vitambulisho vya wasio na kazi hawatoi. Kukosa kazi ni kosa la jinai na wengi wako ndani kwa kosa hilo. Tunaendelea kuzama na wenzetu wameokoa taaluma zao za kisiasa zilizokuwa hatarini kuzama. Tunainua mikono yetu watuone ili sasa waonyeshe kweli kama wanaweza kutuokoa. Njoni mtutoe kwenye dimbwi hili la umaskini. Ndiyo mnasema tufanye kazi kwa bidii sawa. Ziko wapi kazi zenyewe? Sanaa na wasanii Imebainika kwamba wale wanaouza kanda bandia za muziki watachukuliwa hatua kali za kisheria watakapobainika. Hii ni kufuatia ongezeko la kutisha la wahuni wanaojihusisha na biashara haramu ya kuuza kanda bila kibali cha wasanii husika. Ni kutokana na hawa wanaouza kanda bandia, ndio maana kiwango cha muziki kimeshuka. Wasanii wengi wameshindwa kurudi studio kurekodi toleo jingine kutokana na wizi wanaofanyiwa mchana jua likiwaka. Ni matumaini yetu kwmba vyombo vinavyohusika vitaliangalia kwa makini suala hili. Wasanii wanaumia na kuteseka, huku wahuni wachache wakijitajirisha kwa jasho la wenzao. Tena kuna mtindo uliozuka siku hizi wa watu kujiita maprojusa, kumbe ni matapeli wanaowarubuni wasanii kwa pesa kidogo ili wapate haki ya kuuza kazi za wasanii hao bila kuwalipa ipasavyo. Inasikitisha kuona kwamba hata REDIO HABARI MAALUM inajihusisha na hujuma hizo.Inaweka gharama za kurekodi muziki katika redio yao ziwe kiwango cha juu sana. Wasanii wanaposhindwa kulipa gharama hizo, wanalazimishwa kuingia katika mikataba feki ya kiutapeli. Kabla wajue nini kinaendelea wanazikuta nyimbo zao zikiuzwa afrika ya mashariki na kati bila wao kupata chochote. Tunalaani wizi huu kwa nguvu zetu zote. Wakati umefika kwa wasanii hasa wa nyimbo za injili, wakatae kunyanyaswa na wasimamie haki zao. Wasipoamka hakuna mwingine wa kuwatetea kama si wao wenyewe. Ukimwi na uchumi Afrika Nchi nyingi za Kiafrika zinakabiliwa na tishio la kuzorota kwa uchumi. Hii ni kutokana na vifo vingi vinavyotokea barani humo, na vingi vinahusishwa moja kwa moja na UKIMWI. Kulingana na mila na desturi za Kiafrika, mtu anapokufa, basi ndugu jamaa na marafiki huacha kila shughuli na kuanza maombolezo ya muda mrefu. Katika maombolezo kama hayo pesa nyingi hutumika kuwalisha waombolezaji, na ngombe kuku na mbuzi huchinjwa wakati wa maombolezo. Wadadisi wanasema kutokana na idadi kubwa ya vifo vinavyotokea siku hizi itabidi waafrika walitizame upya suala la maombolezo yenye gharama nyingi. Tuendako, Mbuzi,kuku na ngombe wa kuchinjwa watamalizika, na hatujui mazishi ya siku za usoni yatakuwa ya jinsi gani. ILa kutokana na dini ya kiislamu kuota mizizi Afrika, wengi wameanza kuzika kiislamu ambapo mtu akifa anazikwa mapema iwezekanavyo kuepusha gharama kubwa ya mazishi. Hata wakristo wengi wameanza kufuata mkondo huo kwani maji yakizidi unga hakuna jinsi. Wengi wanasema juhudi kubwa zinatakiwa zielekezwe katika kuwatibu na kuwaonyesha upendo wagonjwa wanapokuwa hai, badala ya kungoja waage dunia na kuanza unafiki wa kuomboleza kwa gharama za juu kuliko zilizotumika kuwatibu walipokuwa wagonjwa. Hata biblia inatufundisha kwamba ni afadhali mbwa mzee aliye hai, kuliko simba kijana aliyekufa. Mtu akiisha kufa, FAILI yake duniani na mbinguni inakuwa imefungwa. Haijalishi wanadamu watafanya nini, lakini haitabadili ukweli kwamba ameenda, nasi tunasubisi siku yetu ya kumfuata alikokwenda. Mtu akienda Amerika ni ajabu kubwa kwani wengi wetu huenda tusifike Amerika wakati wa uhai wetu. Lakini mtu akifa siyo ajabu kwani sote siku moja tutakufa. Nalo neno la Mungu katika kitabu cha mithali 5:15-22 linasema ifuatavyo: Unywe maji ya birika lako mwenyewe, Na maji yenye kububujika katika kisima chako. Je! chemchemi zako zitawanyike mbali, na mito ya maji katika njia kuu? Yawe yako mwenyewe peke yako, Wala si ya wageni pamoja nawe. Chemchemi yako ibarikiwe; Nawe umfurahie mke wa ujana wako. Ni ayala apendaye na paa apendezae. Maziwa yake yakutoshe siku zote. Na kwa upendo wake ushangilie daima. Mwanangu mbona unashangilia malaya, na kukikumbatia kifua cha mgeni? Kwa maana njia za mwanadamu zi mbele za macho ya Bwana. Na mienendo yake yote huitafakari. Maovu yake yeye yatampata mdhalimu, Naye atashikwa kwa kamba za dhambi zake. Dar es salaam Kanisa la Full Gospel Bible Felloship linaloongozwa na Kakobe limeitisha mkutano wa wachungaji wa kipentekoste Tanzania nzima. Lengo la mkutano huo imeelezwa kwamba ni kuweka mikakati ya kujenga mahusiano mazuri kati ya kanisa na serikali. Akizungumza wakati wa ufunguzi, Mwenyekiti wa umoja huo Askofu Sylvester Gamanywa alisema, wakati umefika kwa serikali kutowapuuza wapentekoste. Alidai kwamba wapentekoste hawapewi nafasi katika vyombo vya habari vya kitaifa jambo ambalo alisema limechangiwa na dhana potovu kwamba walokole ni watu waliochanganyikiwa kimaisha na hawana lolote la kuweza kuisaidia serikali kiutawala. Naye Askofu Kitonga wa kanisa la Redeemed Kenya alisema anaunga mkono kongamano hilo na akasema anafurahi kuona askofu Kakobe akiufuata ushauri wake wa kutoipinga serikali iliyoko madarakani. Aliongeza kwamba nchini Kenya serikali iliyokuwa madarakani ilitambua umuhimu wa wapentekoste na iliwatumia sana katika kuwasilisha sera za serikali kwa wananchi ambao wengi ni washirika wa makanisa hayo. Lakini wale wanaopinga wazo la kanisa kununuliwa na serikali wanasema, Kanisa ni chombo cha kukemea maovu katika jamii na serikali ikiwa mojawapo. Waliongeza kwamba Kanisa linapokubali kununuliwa na serikali, hiyo ni hatari kubwa. Walisisitiza kwamba Inasikitisha kuona kwamba kanisa la Tanzania limekubali kununuliwa na serikali ya CCM ambayo sifa yake ni kuwaua raia wasiokubaliana na sera zao mbovu za wizi , Ukandamizaji, na uonevu wa kila namna kwa raia wa Tanzania. Mungu lisaidie kanisa lako Tanzania. Nairobi Kufuatia kifo cha aliyekuwa makamu wa rais Mheshimiwa Maiko Wamalwa Kijana, upepo wa kisiasa nchini Kenya umebadili mkondo wake. Sasa kila sikio limeelekezwa kusikia nani atakayechaguliwa kushika nafasi ya makamu wa rais. Wengine wanasema lazima karata ya ukabila ifuatwe na makamu wa atoke Uluyani, na kuna wale wanaosema sasa ni wakati wa wa kuweka ukabila pembeni na kumchagua yeyote anayeweza kuishikilia nafasi hiyo hata kama hatoki Westani Kenya. Saitoti anaonekana na wengi kuwa na uzoevu wa kazi hiyo japo kuna dosari ndogo ndogo. Wengine wanasema kuwa Mudi Awori anafaa kikabila hata kama hana uzoevu. Wanadai kwamba mtu hawezi kuupata uzoevu kabla hajaanza kazi yenyewe. Liberia Aliyekuwa rais wa Laiberia Charles Tailor amekubali kuihama nchi yake, ili akaishi uhamishoni nchini Nigeria. Hii ni kufuatia shinikizo alilowekewa na nchi za magharibi zikiongozwa na Amerika. Kwao Tailor akiondoka Liberia, matatizo ya vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Liberia yatakwisha. Swali ambalo wengi wanajiuliza ni kama Tailor ndiye aliyekuwa tatizo Liberia. Wachunguzi wa mambo wanadadisi kwamba Amerika ndio wamekuwa wakichochea vita katika nchi nyingi za kiafrika kwa lengo la kulinda maslahi yao katika bara hili. Tunasubiri kuona raia wa Liberia wakiishi kwa amani bila au na Tailor mradi tu yawe ni matakwa yao na siyo shinikizo kutoka Marekani. Nairobi Mzozo mkubwa uliokikumba chama cha tawala Nack unatishia kukisambaratisha chama hicho kama hatua za haraka hazitachukuliwa kukinusuru chama. migawanyiko imejitokeza baada ya wanachama wa muungano huo kudai kwamba makubaliano yaliyowaleta pamoja yameanza kukiukwa. Suala lililozua utata zaidi ni lile la waziri mkuu nafasi aliyoahidiwa mheshimiwa Raila Odinga. Wengine wanasema hawakukubaliana hivyo, na kuna wale wanaokubali lakini wanasema waziri mkuu hatakiwi kuwa na uwezo kuliko rais. Hakuna atakayepinga kwamba tofauti hizo zimekitikisa chama cha Narck ambacho kiliingia mararakani kwa kishindo na kukitoa madarakani chama cha KANU ambacho mpaka sasa hakijayaamini macho yake kwamba kimewekwa benchi. Naye mbunge wa Nakuru akiwaonya wakereketwa wa nafasi ya waziri mkuu, alitoa maneno yenye cheche za moto pale alipowakumbusha kuhusu kuuawa kwa mwanasiasa mashuuri Tom Mboya. Alieleza sababu zake ambazo wengi wamezitafsiri kama matisho. Wengi wanajiuliza ikiwa Tom Mboya wakati wa Kenyatta na Ouko wakati wa Moi walikutana na vifo vyao katika mazingara ya kutatanisha, je nani anayeweza kufuatia? Mungu apishe mbali. Ni maombi yetu wakubaliane kutimiza makubaliano yao ya awali kuepusha shari. Mungu ibariki Kenya. Makanisani Redio Biblia husema FM ambayo hutangaza katika megahads 90.9 katika viunga vya Nairobi na megahads 96.9 katika Machakos na mkoa wa kati sasa haiko hewani. Hii ni kufuatia msako uliofanywa na maofisa wa forodha katika kituo hicho na kungoa mitambo ya kurushia matangazo kwa kile walichokiita kwamba mitambo hiyo haijalipiwa ushuru. Japo mitambo midogo ya 90.9 Nairobi haikuchukuliwa, lakini ile iliyokuwa ikiwawezesha kusikika mkoa wa kati na bonde la ufa yaani Nakuru Eldoret hadi Bungoma Imezimwa. Hii ni stesheni ya kwanza kuzimiwa mitambo yake ya kurusha matangazo tangu kuundwa kwa serikali mpya. Wakati wa serikali ya zamani, Redio CITIZEN na TV yao ndiyo ilikuwa ikifungiwa kila kukicha. Lakini sasa ndio wanaotamba kila kona ya nchi. Redio CITIZEN Bila kuona haya, wakati wa uchaguzi mkuu walikipigia debe chama cha Narc na kazi yao ilizaa matunda pale Narc iliposhinda kwa kishindo na kuunda serikali mpya. Wakati huo ilisifika kwa kuikosoa serikali, na sasa inasifika kwa kuisifia serikali. Wengi wanajiuliza kama sasa ni zamu ya Redio ya injili Biblia husema FM kuzimiwa mitambo yao kama CITIZEN wakati huo? Tunaomba isiwe hivyo. Hasa wakati huu ambao serikali inaweka huru masafa ya kutangaza. Ni matumaini yetu kwamba vyombo vya habari vitakuwa huru kuliko mwanzoni, lakini siyo kwa ishara tunazoanza kuziona. Mkurugenzi wa redio hiyo amesema kwamba walipewa barua ya kuwawezesha kukwepa kulipa kodi kwani redio yao ni chombo cha kuhubiria Injili na wala siyo kwa ajili ya biashara. Redio hiyo inamilikiwa na kanisa la AIC ambalo rais mstaafu Daniel Arap Moi ni mshirika wake. Rais aliyeko madarakani kwa sasa ni mshirika wa kanisa katoliki na tayari kanisa hilo lina redio yenye mitambo ya nguvu. Yao haijazimwa, kwa nini wengine wazimiwe. Hayo ndiyo maswali ya walio wengi. Amerika Makanisa ulimwenguni yamegawanyika kuhusu suala la kutawazwa uaskofu askofu shoga wa kimarekani. Kwa mara ya kwanza Amerika inataka kutumia nguvu yake ya kushawishi duniani ili dunia ikubaliane na ushoga, na sasa wanataka ikubaliwe kanisani. Tunawaunga mkono wote wanaoupinga uovu huu kwa nguvu zao zote. Na hii inathibitisha kwa mara nyingine kwamba Amerika siyo wakristo kama wanavyotutaka tuamini. Mmomonyoko wa maadili duniani umesababishwa zaidi na Amerika wakitumia sana vyombo vya habari na sanaa ya filamu zao chafu, na sasa wanataka kulitumia kanisa kusambaza uchafu wao kwa kisingizio cha uhuru wa kuamua. Tunasubiri kusikia misimamo ya makanisa kuhusu suala hili.
Tangaza
Biashara yako Bure Bonyeza
hapa usome zaidi |
||||||||||||
|
|
|
|